Serikali imetoa onyo kwa baadhi ya watu wanovunja sheria kwa kuvamia maeneo ya watu na ya umma katika kipindi cha chaguzi wakitegemea hawatachukuliwa hatua na kuonewa huruma na watawala.
Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, wakati wa ziara ya kufuatilia maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu migogoro ya vijiji 995 nchini.
Silaa amewataka viongozi na watumishi wa umma, kusimamia sheria za umiliki wa ardhi bila kusita kwa watu wote wanaozalisha migogoro kwa kujiingiza kwenye maeneo ya watu na maeneo ya hifadhi kisa wataonewa huruma na viongozi kwasababu ni kipindi cha uchaguzi.
Ameongeza kuwa mwaka 2024 na 2025 ni miaka ya uchaguzi hivyo wananchi wasijiingize kwenye uvamizi wa ardhi za watu kiholela kwa kutegemea huruma ya sheria jambo ambalo baadae husababisha migogoro.