Kikosi cha Mabingwa watetezi Tanzania Bara Young Africans Kimeongia kambini leo Jumatatu (Desemba 11) kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa Jumamosi (Desemba 16) katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Young Africans walirejea nchini alfajiri ya kuamkia jana Jumapili (Desemba 10) wakitokea Kumasi, Ghana ambapo walitoka sare ya bao 1-1 na Medeama kwenye mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Afisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe amesema kwa sasa akili na mawazo yao wanaelekeza kwenye mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar kuhakikisha wanachukua pointi tatu na kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi.
“Mawazo yetu kwa sasa ni kuchukua pointi tatu dhidi ya Mtibwa Sugar, lengo nikirudi kileleni mwa msimamo wa ligi, na baada ya hapo ndio tutaamza kuupigia hesabu mchezo wetu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Medeama ambao tutacheza nao Desemba 20,” amesema Kamwe.
Kamwe amesema Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ametaka timu iingie mapema kambini bila kujali udhaifu wa wapinzarni wanaotarajia kukutana kwamba watashinda kirahisi.
Amesema anachojua yeye hiyo ni mechi ngumu na inahitaji maandalizi ya kutosha ili kuendeleza pale walipoishia kabla hawajaanza kucheza mechi za makundi.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, Young Africans ipo nafasi ya pili wakikusanya pointi 24 katika michezo tisa wakati vinara ni Azam FC yenye pointi 25 na michezo 11.