Timu ya taifa ya Ghana, Black Stars’ itaanza maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ kwa kuweka kambi mjini Johannesburg, Afrika Kusini kuanzia juma lijalo.
Shirikisho la soka nchini Ghana (FA) limethibitisha kuwa kikosi cha timu yao ya taifa kinachotamba na historia ya kutwaa ubingwa wa Afrika mara nne, kitakutana Jumapili kuanza kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini kabla ya fainali za mwezi ujao nchini Ivory Coast.
Ghana itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana Januari 08 kabla ya kusafiri kwenda Abidjan siku mbili baadae.
Kocha wa Black Stars, Chris Hughton amethibitisha kuwa mazoezi katika kambi ya Johannesburg vyombo vya habari na umma hawataruhusiwa.
Timu ya Hughton ipo Kundi B pamoja na miamba Misri, Cape Verde na Msumbiji.
Wataanza kampeni yao dhidi ya Cape Verde Januari 14 na watarudiana katika mehi ya Kombe la Dunia mapema mwaka huu.
Ghana itacheza na washindi mara saba wa AFCON, timu ya Misri Januari 18 katika pambano hilo gumu kati ya vigogo hao wa juu wa soka Barani Afrika.
Black Stars watahitimisha mechi zao za makundi dhidi ya Msumbiji Januari 22.
Hughton anatarajiwa kutaja kikosi imara ikiwa ni pamoja na kiungo wa kati wa Arsenal Thomas Partey na nyota wa West Ham, Mohammed Kudus.
Nahodha Andre Ayew ataongoza kikosi hicho wakati akitazamia kuihamasisha Ghana kushinda AFCON kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1982.
Ikiwa na jumla ya mataji manne, Ghana inataka kuziba pengo la Misri na Cameroon katika rekodi ya kushinda mataji matano ya AFCON.
Baada ya kutolewa hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2022, Ghana wanafanya marekebisho katika mechi za Ivory Coast lakini wapo kundi gumu na Hughton anajua kikosi chake kinakabiliwa na mtihani mkali.
Kocha huyo anatumai kambi ya mazoezi ya Johannesburg itaisaidia Ghana kupata kiwango bora kabla ya kuanza kwa AFCON 2023.