Kiungo Mshambuliaji Hakim Ziyech mkataba wake wa mkopo huko Galatasaray unaweza kuvunjwa ndani ya mwezi huu wa Januari kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa wakati ananaswa kutoka Chelsea.

The Blues ilimtoa kwa mkopo mkali huyo wa Morocco wakati wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, kujaribu kumpeleka sehemu ambako atapata muda wa kucheza baada kukwama Stamford Bridge.

Lakini, tangu alipotua Galatasaray mambo yamekwenda tofauti kabisa kwa Ziyech mwenye umri wa miaka 30, akipata majeraha ya mara kwa mara na kumtibulia muda wake wa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

Ziyech amecheza mechi tisa tu katika ligi ya msimu huu, huku kwenye mechi hizo ameanzishwa mara sita.

kwa mujibu wa NTV Spor, staa huyo wa zamani wa Ajax anaweza kujikuta akitemwa na Galatasaray kwenye dirisha hili la Januari licha ya mkopo wake kufika tamati mwisho wa msimu.

Kwa muda ambao amekuwa kwenye kikosi hicho cha Istanbul, Ziyech amefunga mabao manne na asisti mbili katika michuano hiyo, lakini amekuwa na wakati mgumnu wa kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Kama mkopo wake utasitishwa na kurudi Chelsea, kuna nafasi finyu ya staa huyo kwenda kupangwa na kocha Mauricio Pochettino, hivyo The Blues itatafuta timu nyingine ya kumpeleka.

Hata hivyo, Ziyech kwa sasa akili yake haipo kwenye soka la klabu, akifikiria zaidi soka la kimataifa ambapo timu yake ya Morocco inajiandaa na michuano ya AFCON 2023 itakayofanyika Ivory Coast.

Che Malone: Tunapaswa kuacha dharau
Chelsea yaingia anga za Man Utd