Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewataka wanafunzi wa Vyuo Vikuu Mkoani hapo kuwa na matumizi sahihi ya vifaa vya mawasiliano ikiwemo simu janja, ili kujiepusha na makosa ya kimtandao.
Wito huo umetolewa na Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Kudhibiti Makosa ya Kimtandao (Cyber crime), wakati wakitoa elimu kwa wanafunzi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro – MUM, kuhusu matumizi sahihi ya Mitandao.
Mtaalam kutoka Kitengo cha makosa ya kimtandao Ofisi ya Upelelezi, Koplo Ayoub Kanick alieleza kuwa watumiaji wanapaswa kuzifahamu sheria za mtandao, kwa kuwa dunia ipo katika kipindi cha utandawazi.
Aidha, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Pendo Meshurie ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la Jinsia Wilaya ya Morogoro alisema, ukatili wa Mitandaoni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia umetajwa kushika kasi na elimu kwa Wanafunzi hao itawasaidia kutambua na kuchukua tahadhari juu ya ukatili huo.
Naye Konsteble Suleyman Mussa toka Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto, alitumia fursa hiyo kueleza maana ya ukatili na aina zake na kuwataka wale wote wanaofanyiwa ukatili kufika katika ofisi za Dawati haswa wanaume ambao muitikio wao bado hauridishi ili waweze kusaidiwa.
Aidha, Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro MUMSO kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Vyuo imelishukuru Jeshi la Polisi huku wakiomba kuwepo muendelezo wa semina mbalimbali zinazohusiana na ulinzi na usalama.