Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, iliyopo Wete imemhukumu kifungo cha miaka 10 Saleh Ali Sultan (37), kwa makosa mawili ya kutishia maisha na shambulio la kudhuru mwili.

Akisoma hukumu, Hakimu wa Mahakama hiyo Asya Ali Abdalla alisema kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili Mahakama imetoa adhabu kwa mshitakiwa kwenda chuo cha mafunzo miaka 7 kwa kosa la kutishia maisha na miaka 3 kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili ikiwa ni adhabu za pamoja na kulipa fidia ya shilingi 500,000.

Akijitetea mbele ya Mahakama, mshitakiwa aliomba apunguziwe adhabu au impe kifungo cha nje cha kutumikia jamii kwani analea watoto ambao mama yao wameshaachana lakini pia anaumwa na mgongo ombi ambalo halikuzingatiwa.

Awali, ilidaiwa kuwa Agosti 28, 2023 majira ya saa 8:44 mchana huko Pandani, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba bila ya halali na kwa dhamira ya kutaka kutenda kosa la shambulio la hatari kwa kutumia kisu, alijaribu kumtishia maisha Sajenti Rashid wa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kaskazini Pemba, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Katika kosa la pili, ni shambulio la kudhuru mwili lililo kinyume na kifungu cha 230 cha kanuni ya adhabu, sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa, siku hiyo Agosti 28, 2023 majira ya saa 8:45 za mchana huko Pandani mshitakiwa alimshambulia askari Polisi mwenye cheo cha konstebo Edward wa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kumjeruhi katika vidole vya mkono wake wa kulia kwa kutumia kisu na kumsababishia jeraha jambo ambalo ni kosa kisheria.

Jenerali agomea upatanisho, adaiwa kutaka vifo zaidi
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 6, 2024