Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati wa mlipuko wa mabomu uliowahi kutokea Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, alimuarifu Rais wa Kipindi hiko Dkt. Jakaya Kikwete juu ya azma yake ya kujiuzuru nafasi ya Waziri wa Ulinzi lakini alikataa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati akiongea na Baraza la Mawaziri baada ya kufanya mabadiliko madogo ya Mawaziri na kuongeza kuwa mabadiliko ni sehemu ya uwajibikaji na kujiuzuru hakutokei kwa muhusika kutenda kosa bali kwa ajili ya tatizo lililojitokeza hata kama hakuhusika.
Amesema, “leo nikwaambieni jambo ambalo sijawahi kulisema, yalipotokea ajali ya mabomu kule Gongo la Mboto, mimi nikiwa Waziri wa Ulinzi nilimpelekea ujumbe kwa Rais wangu wakati ule alikuwa Mheshimiwa Kikwete nikimtaka aridhie nijiuzulu, lakini sikukurupuka kwenda kutangaza kwenye vyombo vya Habari nikatangaza kwamba nimejiuzuru si utaratibu.”
“Utaratibu unataka umwambie aliyekuteuwa akikubali ndio ukatangaze, Mheshimiwa Kikwete akasema hii ni ajali na huna sababu ya kujiuzuru, hakuna mtu alisikia kama nilitaka kujiuzuru leo nasema hili hadharani sijawahi kulisema. kwa hiyo kujiuzuru ni njia ya kuwajibika,” alifafanua Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.