Kikosi cha Simba SC leo Ijumaa (Februari 23) itakuwa ugenini nchini lvory Coast kuikabili Asec Mimosas katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, katika Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny mjini Abidjan-Ivory Coast kuanzia saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Miamba hiyo ya soka ya Tanzania, Simba SC itaingia kwenye mchezo wa leo ikihitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali.
Wenyeji Asec Mimosas wapo kileleni mwa msimamo wa Kundi B wakikusanya Pointi 10 katika michezo minne iliyopita wakati Simba SC ipo nafasi ya pili wakiwa na Pointi tano katika idadi kama hiyo ya mechi.
Katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, timu hizo zilitoka sare kwa kufungana bao 1-1, Saido Ntibazonkiza akifunga bao la kuongoza kwa mkwaju wa Penati dakika ya 44 kabla ya Serge Pokou kuisawazishia Asec Mimosas dakika ya 77.
Pamoja na Asec tayari kujihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali, mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na upinzari mkali kwani watahitaji kushinda ili kumaliza kileleni mwa kundi hilo ili kupangiwa timu itakayoshika nafasi ya pili kutoka kundi lingine.
Kujiweka kwenye mazingira ya kuungana na Asec hatua ya Robo Fainali na kuziacha timu za Wydad Casablanca na Jwenang Galaxy, ambazo nazo zina nafasi ya kuingia hatua hiyo, Simba SC ni lazima kupata ushindi kwenye mchezo wa leo.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha akiuzungumzia mchezo wa leo amesema mazoezi ya siku mbili waliyoyafanya tangu wafike Ivory Coast, yamewafanya kuwa tayari, huku lengo kuu ni kupata Pointi tatu zitakazofufua matumaini yao ya kwenda Robo Fainali.
“Ni mchezo mgumu, tunalijua hilo sababu tunacheza na timu bora na vinara kwenye Kundi letu, lakini tupo tayari, vijana wangu wamenihakikishia ushindi, tutamkosa Willy Onana na Kipa Ayoub Lakred lakini tumekuja na wachezaji 22 ambao naamini watatupa ushindi,” amesema Benchikha.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Asec Mimosas, Julien Chevalier amesema pamoja na mazingira mazuri waliyopo lakini lengo lao kuu ni kushinda mchezo huo, na kumaliza nafasi ya kwanza lakini pia kutengeneza rekodi na kumbukumbu nzuri siku zijazo.