Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu amesema kuwa klabu hiyo haijauzwa tofauti na alivyonukuliwa Rais wa heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ kudai kuwa aliinunua timu hiyo miaka mitano iliyopita.
Mangungu ametoa ufafanuzi huo jijini Dar es salaam kwa kusema hakuna kitu kama hicho, na klabu ya Simba SC haijawahi kuuzwa na haitakuja kuuzwa.
“Simba SC ipo, kitu ambacho kimejitokeza ni kwamba nadhani uelewa wa watu wengi hata wana Simba wenyewe kuhusu mabadiliko yaliyofanyika ndani ni mdogo.
“Simba SC kama ilivyo kwa timu nyingine ilikuwa inaendeshwa kwa mfumo wa ridhaa baada ya mabadiliko ya maendeleo na changamoto nyingi za kiuendeshaji Mohamed Dewji ni mmoja watu waliojitolea sana kuisaidia klabu,” amesema Mangungu
Amesema Dewji kipindi ambacho hakuwa sehemu ya Simba SC alikuwa anatoa michango yake kama watu wengine wanaochangia, lakini baadae akatoa wazo la kutengeneza mfumo ambao watawekeza ili klabu iwe ya kiushindani zaidi.
“Hivyo kwa makubaliano ya awali tuliunda chombo ambacho kiliitwa Simba SC Company Ltd, ambayo ndio imegawanya muundo wa shea (hisa) wa asilimnia 51/49 mwanzoni ilikuwa 50/50.
“Lakini masharti yaliyowekwa na serikali yalilazimisha kuwa lazima upande wa wanachama uwe wenye hisa nyingi chombo hicho kipo na kwa uelewa wangu na ndivyo ukweli ulivyo,”