Wakati Simba SC ikijichimbia Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, Benchi la Ufundi la timu hiyo limedai kuwa kambi hiyo itawasaidia kukiandaa vyema kikosi chao kuwatoa wapinzani wao hao.
Simba SC itachuana na Al Ahly ljumaa (Machi 29) katika mchezo wa mkondo wa kwanza utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam huku ikihitajika kuutumia vyema uwanja wake huo wa nyumbani kabla ya kwenda ugenini.
Kocha msaidizi wa Simba SC, Suleimani Matola amesema kikosi chao kimeamua kuweka kambi visiwani humo kupata muda mzuri wa kujiandaa na mchezo huo wa aina yake.
Matola amesema timu yao inahitaji utulivu mkubwa, hivyo anaamini kambi hiyo itawafanya wajiandae vizuri kimbinu na kiufundi kuwa bora dhidi ya Al Ahly.
“Tunajua utakuwa mchezo mgumu ila lengo letu kubwa ni kuona tunashinda, ndiyo maana tumeona tuweke kambi Zanzibar kwani tutapata utulivu na muda mzuri wa kupanga mbinu kuhakikisha tunashinda mchezo wetu,” amesema
Matola ameweka wazi kuwa, wachezaji wao ambao wapo katika majukumu yao ya timu za taifa watajiunga na kambi baada ya kalenda ya mechi za kimataifa za Shirikisho la Soka la Kimataifa ‘FIFA’ kumalizika.
Kocha huyo amesema wakiwa Zanzibar watacheza mechi mmoja ya kirafiki kupima uwezo wao kabla ya kuvaana na Al Ahly.
Ikiwa Wekundu hao wa Msimbazi wataitoa Al Ahly watatinga Nusu Fainali kucheza na mshindi kati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Petro de Luanda ya Angola.
Simba ilitinga hatua ya Robo Fainali baada ya kushika nafasi ya pili katika Kundi B ikiwa na alama tisa nyuma ya kinara ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyovuna alama 11.