Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.

Katika kuadhimisha siku ya Afya ya Kinywa na Meno, Wananchi zaidi ya 6,000 wamejitokeza kupata huduma hiyo kutoka kwa wataalamu wa afya ya Kinywa na Meno zaidi ya 80 Mkoani Pwani, katika kipindi cha wiki moja huku Wananchi wakishauriwa kutunza afya ya mwili mzima kwani upo uhusiano mkubwa kati ya afya ya meno na afya ya mwili.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Kibaha, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Nchini – TDA, Dkt. Gema Belege amesema Wataalamu hao ni kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili na wapo kwa ajili ya maadhimisho ya siku hiyo Duniani, ambayo huadhimiswa kila Machi 20 ambapo kitaifa yanafanyika mjini Kibaha.

Amesema, Wataalamu hao wamekuwa na kambi tatu katika vituo vya huduma katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, Hospitali ya Wilaya ya Lulanzi na katika Kituo cha afya cha Mkoani.

“Lakini pia tunetembelea shule za msingi tisa, vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu saba ambako tumetoa elimu na kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno na waliobainika kuhitaji matibabu tumewapeleka kwenye kambi za afya hizi tatu kwaajili ya kupatiwa huduma za afya,” amesema Dkt. Gema.

Kuhusu tatizo waliloliona kwa Watafuta huduma, amesema wengi wao wana tatizo la ugonjwa wa kuoza meno, magonjwa ya fizi, mpangilio mbaya wa meno na ukosefu wa meno au mapengo na kwamba wamewapa elimu ya afya ya Kinywa na Meno, matibabu ya kuziba na kusafisha meno.

Dkt. Gema ameongeza kuwa, “mpaka leo tumeweza kutoa meno bandia bure kwa wagonjwa zaidi ya 133 yaani Wananchi wote waliopata huduma kwenye maadhimisho haya wamepata huduma bila malipo yoyote na tumewaambia iwapo watatunza afya ya kinywa na meno vizuri pia kutunza afya ya mwili mzima maana Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya meno na afya ya mwili.”

Hata hivyo, ameshauri kuwa, “kama mtu ameona tatizo lolote la afya ya kinywa na meno asiende kwenye duka la dawa akaanza kutumia madawa kwa kupokea maelekezo yasiyoyakitaalamu bali waende kwa Wataalamu ili wakawachunguze, kuwashauri na kuwapa tiba sahihi kwasababu vifaa vipo na Wataalamu pia wapo.”

Simba SC yatambia kambi ya Zanzibar
Siku 123 za ulinzi wa penzi kwa Mnyororo zatamatika kwa usaliti