Kikosi cha Simba SC kinatarajia kuelekea Cairo, Misri kesho Jumatano (Aprili 03) kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, Uwanja wa Cairo International Ijumaa (Aprili 5).

Simba SC ambao walifungwa bao 1-0 katika mhezo uliopita Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Ijumaa (Machi 29) watahitaji ushindi kuingia Nusu Fainali ya michuano hiyo.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema walianza mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo juzi Jumapili (Machi 31) na kwamba kesho Jumatano watasafiri kuelekea Cairo, Misri kuwavaa mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi kitaondoka kesho Jumatano (Aprili 03) kwenda Cairo. Tutaenda kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ya kutuvusha,” amesema Ahmed.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Abdelhak Benchikha amesema wanakwenda Cairo na dhamira moja ya kuleta furaha kwa mashabiki kwani bado wanayo nafasi na kusema pamoja na ubora wa kikosi cha Al Ahly lakini wanafungika.

“Malengo ni Simba SC kwenda Nusu Fainali, tulipoteza kutokana na makosa yetu wenyewe. Washambuliaji walikosa umakini lakini tumerekebisha kila kitu ili tupate matokeo nzuri ugenini,” amesema Benchikha.

Simba SC ndiyo timu pekee iliyopoteza mchezo hatua ya Robo Fainali huku timu nyingine zote zikitoka sare ya bila kufungana.

Mara ya mwisho Simba SC kucheza Nusu Fainali ya michuano hiyo ilikuwa ni mwaka 1974 michuano ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika ikifungwa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa Penati 3-0 baada ya kila moja kushinda mchezo wa nyumbani kwa bao 1-0.

Rekodi zinaonesha Simba SC haijawahi kupata ushindi ugenini mbele ya Al Ahly kwani mechi nne zilizopita ikiwamo moja ya Kombe la Washindi mwaka 1985 na mbili za makundi ya Ligi ya Mabingwa walifungwa zote na moja ya michuano mipya ya Ligi ya Soka ya Afrika ilitoka sare ya bao 1-1.

 

 

MALIMWENGU: Mapepe yalivyoniingiza matatani
Shambulizi la Moscow: Wengine wanne mbaroni