Wakati Azam FC ikiendelea na maandalizi ya mechi zake za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (Kombe la CRDB BANK), Kocha Youssouph Dabo ametamba mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar utaonyesha ni jinsi gani timu yake itakavyorejea ikiwa na makali mapya.

Azam FC inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa Jumapili (Aprili 07) katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara (Kombe la CRDB BANK) utakaochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha Dabo amesema mchezo dhidi ya Mtibwa ni muhimu kwao kushinda lakini pia utamsaidia kujua ubora wa timu yake baada ya kufanya maandalizi ya muda mrefu.

Amesema mchezo huo ndiyo utatoa taswira ya jinsi gani kikosi chake kilivyoweza kujifua katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama.

“Tumekuwa na mazoezi ya muda mrefu ya kujiandaa na tumerekebisha mapungufu yaliojitokeza katika mechi zilizopita pia mechi za kirafiki ambazo tulizocheza zitatusaidia kurejesha kiwango kizuri kwa wachezaji wangu, hivyo mechi yetu na Mtibwa Sugar ndiyo itaonyesha taswira halisi ya kikosi changu,” amesema Dabo.

Kocha huyo huyo amesema baada ya kumalizana na Mtibwa Sugar atakuwa na kibarua kikubwa katika mechi zake za Ligi Kuu lakini halitampa hofu kwani zilizokuwa mbele yao, amejipanga kushinda mechi zote kuikaribisha Ihefu FC April 27 mwaka huu.

Amesema baada ya kumalizana na Mtibwa Sugar atarejea katika ligi huku akiwa na mchezo ugenini dhidi ya Namungo FC ugenini April 13, kabla ya kurejea nyumbani kumenyana na Mashujaa FC April 16, mwaka huu.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 47 imeshinda mechi 14, sare tano na kupoteza michezo miwili baada ya kushuka dimbani mara 21.

FECAFOOT yakana ujio wa kocha mpya
Singapore yachomoa Jumuia ya Madola