Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA imekamilisha ujenzi wa Daraja la Chuma la mto Lwipa (Mabey Bridge) lenye urefu wa mita 27 na matengenezo ya barabara ya Kisegese – Chiwachiwa – Lavena yenye urefu wa Km 15 kwa gharama za shilingi bilioni 1.8.
Kukamilika kwa daraja hilo limewezesha kuunganisha Kata ya Mbingu na Namwawala katika Halmashauri ya Mlimba, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero, Mhandisi Sadiki Kalumi amesema ujenzi wa Daraja hilo lililojengwa na wataalam kutoka TARURA litarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.
Amesema, “Daraja hili lina urefu wa mita 27 limegharimu shilingi milioni 900, lakini pamoja na Daraja kuna matengenezo ya Barabara ambayo itajengwa kwa kiwango cha changarawe pamoja na makalavati kwa gharama ya shilingi milioni 900 kufanya jumla ya shilingi Bilioni 1.8.”
Mhandisi Sadiki amesema hapo awali Wananchi walikuwa wakitumia gogo kuvuka kabla ya kujengwa kwa Daraja la mbao ambalo lilikuwa si la uhakika kabla ya TARURA kujenga Daraja la Chuma katika Mto huo na kuchochea shughuli za Kilimo katika maeneo hayo ya Chiwachiwa na Kisegese.
“Wakazi wa maeneo haya wanajishughulisha na Kilimo cha Kokoa, Mpunga, Mahindi, Mawese, Ufuta pamoja na Ndizi hivyo daraja hili ni mkombozi kwani litawaletea maendeleo na kuwainua kiuchumi.”
Diwani wa Kata ya Mbingu, Nestory Kelula amesema wakazi wa Kata ya Mbingu ambao ni wakulima walipata tabu katika kusafirisha mazao yao kutoka Chiwachiwa hadi Kisegese kwa kuwa kulikuwa hakuna mawasiliano hivyo kuwalazimu kusafirisha mazao kwa kutumia baisikeli kwa gharama kubwa na kushindwa kuona thamani ya mazao yao.
Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Kisegese Raymond Samson anasema kukamilika kwa Daraja hilo litawasaidia katika usafirishaji wa mazao yao katika vipindi vyote vya mwaka.