Jeshi la Polisi Nchini, linatalajia kuwa mwenyeji wa zoezi la mafunzo ya utayari kwa vitendo mwaka 2024, litakalojumuisha nchi 14 wanachama wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (EAPCCO) kuanzia Aprili 13–18, 2024.

Akitoa tarifa hiyo hii leo Aprili 11, 2024 Msemaji wa Jesh la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi – DCP, David Misime amesema zoezi hilo la pamoja linatarajiwa kufanyika katika Shule ya Polisi Tanzania – Moshi ambapo takribani Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wapatao 670 wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.

Amebainisha kuwa, kufanyika kwa mazoezi hayo kunatokana na maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Shirikisho la Polisi Ukanda wa Mashariki mwa Afrika katika mikutano yao ya kila mwaka.

Ameongeza kuwa Katika mkutano uliofanyika mwezi Oktoba, 2021 Kinshasa nchini DRC, Wakuu hao wa Polisi walipitisha azimio la zoezi hili kufanyika hapa nchini.

Pia amezitaja Nchi zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na mwenyeji Tanzania, Burundi, Eritrea, Djibouti, DRC Kongo, Kenya, Komoro, Ethiopia, Shelisheli, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudani Kusini na Uganda.

Misime amesema lengo la zoezi hilo na mazoezi mengine yaliyopita ni kuwajengea Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali uwezo wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu unaovuka mipaka kama vile ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, Biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kubadilishana uzoefu na taarifa za kitelejensia.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Aprili 12, 2024
TARURA yakamilisha ujenzi Daraja la Chuma Mto Lwipa