Kamati ya wataalamu wa masuala ya Habari Zanzibar – ZAMECO, imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kufuatilia mchakato wa marekebisho ya sheria za habari ikiwemo sheria ya Utangazaji No. 7 ya 1997, ambayo ilifanyiwa marekebisho na sheria No. 1 ya 2010.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), imeeleza kuwa katika vikao mbalimbali, ZAMECO ilitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria hio kwa lengo la kupatikana sharia mpya na rafiki kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.

Imeeleza kuwa,  Aprili 9, 2024 ZAMECO walifika Afisi za Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar Vuga, kujua hatua iliyofikiwa baada ya kupokea mapendekezo hayo Oktoba 2023, ambapo Mratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Zanzibar, Shifaa Said alisema ufuatiliaji umefanyika, ili kuhakikisha mchakato wa kupata rasimu ya sharia ya Utangazaji unakwenda vizuri na hatimae sheria mpya itayokidhi vigezo vya kihabari ipatikane.

Kwa upande wake, Mwandishi wa Habari Mkongwe, Salim Said alisisema Vyombo vya Habari havina nia mbaya na Serikali, kwani ni washirika muhimu katika kuleta maendeleo kwa jamii hivyo jitihada za ZAMECO na wengine katika kuendeleza maboresho ya sheria ya Utangazaji zinachukuliwa kama sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya habari na serikali.

Alisema, “Vyombo vya habari havina uadui na Serikali, sisi ni washirika wazuri na wenye lengo jema kwa jamii na nchi kwa ujumla, kwa kuzingatia vyombo vya habari ni nguzo ya maendeleo ya uchumi.” huku Katibu Tume ya Kurekebisha Sheria, Mussa Kombo Bakari akiwapongeza ZAMECO kwa jitihada wanazozichukuwa kutafuta maendeleo ya tasnia ya Habari na kubainisha kuwa mapendekezo waliyowasilisha yamepokelewa na kufanyiwa kazi.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa alitoa shukrani kwa Katibu na Wafanyakazi wote wa Tume kwa ushirikiano wao katika mchakato huu wa kupata sheria mpya huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu katika kuhakikisha upatikanaji wa sheria mpya kwa maslahi ya Zanzibar na wazanzibari wote.

Ni takribani miaka 20 sasa Wadau wa masuala ya Habari Zanzibar wamekua wakipambania marekebisho ya sheria mbalimbali za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu No. 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria No. 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Utangazaji No. 7  ya 1997 ambayo ilifanyiwa marekebisho na Sheria No. 1 ya 2010, ambapo Oktoba mwaka jana Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar ilipokea mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya uatangazaji lengo ni kupata sheria huru iliyokua rafiki kwa tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.

Sera mpya ya Mikopo kuwanufaisha Vijana
MAKALA: Mr. Bean: Jiwe lililokataliwa na Waashi