Anaitwa Rowan Atkinson, wengi wanamfahamu kama MR BEAN ukimuona tu unaweza kuanza kucheka kutokana na vitimbwi vyake. Yeye ni ushuhuda tosha wa kutokukata tamaa, ili kutimiza ndoto.

Rowan Atkinson alizaliwa katika familia ya kipato cha kati Januari 6, 1955 huko Consett, County Durham, England na wazazi wake ambao ni Baba Eric Atkinson aliyekuwa Mkulima na Mkurugenzi wa Kampuni, na mama yake Ella May.

Aliteseka sana akiwa mtoto kwa sababu ya kigugumizi chake, kwani alitaniwa na kuonewa shuleni si kwa sababu tu ya hicho kigugumizi, la hasha bali pia sura yake, wakisema anaonekana kituko hivyo alitambulika kama mtoto wa ajabu kitu kilichomfanya awe mwenye haya, aliyejitenga na ambaye hakuwa na marafiki wengi na alipenda sana somo la Sayansi.

Mmoja wa Walimu wake aliwahi kusema hakuna kitu kilicho bora juu yake akidai, “sikutarajia kuwa atakuja kuwa mwanasayansi mahiri, lakini amethibitisha kuwa kila mtu alimkosea kwa kumdhani visivyo”. Baadaye akajiunga katika Chuo Kikuu cha Oxford na huko alianza kupenda uigizaji lakini hakuweza kuigiza kwa sababu ya shida yake ya kuongea.

Akapata shahada yake ya uzamili katika uhandisi wa umeme kabla ya kuonekana katika filamu au kipindi chochote cha televisheni ndipo aliamua kuendeleza ndoto yake na kuwa mwigizaji, hivyo akajiandikisha katika kundi la vichekesho lakini tena, kigugumizi chake kikamkwamisha.

Watengeneza Vipindi wa Televisheni walimkataa na alihisi kukata tamaa lakini licha ya kukataliwa mara nyingi hakuacha kujiamini kwani alikuwa na shauku kubwa ya kuwafanya watu wacheke na alijua kwamba alikuwa fundi sana katika hilo.

Hapo Bean akaona isiwe tabu ndipo alianza kuzingatia zaidi michoro yake ya asili ya vichekesho kwa kugundua kuwa angeweza kuongea kwa ufasaha kila alipocheza tabia fulani akipata njia ya kukishinda kigugumizi chake na kukitumia kama msukumo kwenye uigizaji.

Baadaye kwa kushirikiana na wadau wake alijipa jina la uigizaji ambalo lilikuja mpa umaarufu la Mr. Bean hapo akanza rasmi mfululizo wa vipindi vya ucheshi vilivyorushwa redioni mwaka wa 1979 vilivyoitwa The Atkinson People.

Ilikuwa na safu ya mahojiano ya kejeli na watu wakuu wa hadithi, ambao walichezwa na Atkinson mwenyewe. Mfululizo huu uliandikwa na Atkinson na Richard Curtis, na kutayarishwa na Griff Rhys Jones na ndipo badaye wakaona vitafaa zaidi kwenye Televisheni.

Baada ya masomo ya chuo kikuu, Atkinson alifanya jaribio moja la kipindi cha Televisheni ya Wikendi ya London mwaka 1979 alichokiia Kicheko cha Makopo. Hapo alipata wafuasi wengi zaidi na tangu wakati huo akaonekana kwenye televisheni akiigiza na wasanii mbalimbali.

Alipata mafanikio na maonesho mengine, yalimfanya kuwa maarufu duniani na licha ya vikwazo vyote alivyokuwa navyo kwa sababu ya sura yake na ugonjwa wa kuzungumza (kigugumizi), alithibitisha kwamba hata bila kuwa mwili wa kishujaa au uso wa Hollywood, unaweza kuwa mmoja wa wengi.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, Mr. Bean alikutana na msanii wa vipodozi, Sunetra Sastry wakati akifanya kazi katika Shirika la BBC na wakafunga ndoa Februari 1990. na kufanikiwa kupata watoto wawili. Badaye mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 58, Atkinson alianza uhusiano mpya na muigizaji Louise Ford baada ya kukutana walipokuwa wakiigiza pamoja.

Hapo Louice Ford akamuacha mpenzi wake James Acaster ili aweze kuwa na Atkinson ambaye naye aliamua kutengana na mke wake mwaka wa 2014 na kumtaliki mwaka wa 2015 ndipo walifanikiwa kupata mtoto mmoja.

Ni mmoja wa waigizaji wanaopendwa na kuheshimika duniani, bila shaka hadithi yake hii inakupa hamasa ya kujikubali jinsi vile ulivyo na ukiamini kwamba unaweza hamisha mlima, pia mafanikio yake yanatia moyo kwani yanatufundisha kwamba ili kufanikiwa maishani, mambo muhimu zaidi ni shauku, bidii, na kujitolea.

Usikate tamaa. Hakuna mtu anayezaliwa mkamilifu. Usiogope. Watu wanaweza kutimiza mambo ya kushangaza kila uchao licha ya udhaifu na kushindwa kwao kwa baadhi ya mambo.

Marekebisho Sheria za Habari; Kamati Zanzibar yaongeza kasi ufuatiliaji
Wadau Pombe ya Mnazi waandamana kuiangukia Serikali