Klabu ya Simba SC iko katika nafasi nzuri ya kumtwaa kocha Florent Ibenge, baada ya mwenyewe kuomba kuondoka ndani ya timu ya Al Hilal ya Sudan, huku uongozi wa timu hiyo ukiendelea kupambana kumbakisha.
Wakati hayo yakiendelea, Klabu ya Simba SC iko mbioni kuwasajili wachezaji wawili wa timu ya Hafia FC ya Guinea, Mohamed Damaro Camara mwenye miaka 21, na Ousmane Fernandez ‘Drame’ miaka 23.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo tofauti vya habari za michezo Afrika, zinaeleza kuwa kocha huyo amekaa vikao viwili na mabosi wa Al Hilal wakimweleza kuwa wana imani naye, lakini mwenyewe amesisitiza kuwa anataka kuondoka na sababu kubwa ni kutaka kuifundisha timu inayocheza Ligi Kuu na kupambania mataji.
“Kwenye majadiliano ya hatima yake, viongozi wamemweleza kocha kuwa bado wana imani na utendaji wa kazi yake na wanataka kuendelea naye, lakini ameng’angania kuondoka kwa sababu timu kwa sasa haichezi ligi kutokana na machafuko yanayoendelea nchini Sudan,” vimeeleza vyanzo hivyo.
Licha ya kwamba Al Hilal huenda ikacheza Ligi Kuu Tanzania Bara nchini, baada ya maombi yao kukubaliwa na TFF, lakini kocha huyo bado anaonekana hajaridhika na hilo.
Ibenge anatajwa kuwa kwenye orodha ya wanaotakiwa na Klabu ya Simba na kupewa nafasi kubwa ya kuwa kocha mkuu, baada ya kuondoka Abdelhak Benchikha, huku kitendo cha kuomba kuondoka Al Hilal kikionekana kuwa huenda tayari ameshafikia makubaliano na kabu hiyo.
Hii si mara ya kwa klabu hiyo kumuhitaj lbenge ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na ilibaki kidogo imnase mwaka 2022 lakini ilishindikana na kuangukia, kwa Zoran Maki.
Pamoja na kusala kocha, Klabu ya Simba imepiga hodi nchini Guinea katika harakati za kuwasainisha viungo wawili, Camara na Drame, ambao wanatajwa kuja kuchukua nafasi ya Sadio Kanoute anayedaiwa kuomba kuondoka mwishoni mwa msimu, pamoja na Fabrice Ngoma.
Usajili huo umetajwa ni kwa ajili ya kuimarisha eneo la kiungo, ambapo Camara anacheza nafasi ya kiungo mkabaji, huku Drame akiwa na uwezo wa kucheza namba sita, na nane.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amesema kila kitu kinakwenda vizuri, lakini hivi sasa siyo wakati wa kuzungumzia kitu chochote kuhusu kocha au usajili kwani akili yao ni kusaka nafasi mbili za juu ili msimu ujao warejee kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Tunaleta kocha bora na tutafanya usajili mkubwa safari hii, mashabiki wetu watulie, kwa sasa si wakati wake, kwanza tuungane, tushikamane ili kupate nafasi ya kurejea tena kule tulikozoea,” amesema Ahmed.
Amesema watafanya maamuzi magumu kwa lengo la kuiboresha timu yao na kuahidi kuwafurahisha mashabiki wao kutokana na usajili watakaoufaya.
Amesema watapitia ripoti ya Benchi la Ufundi lililopo chini ya Juma Mgunda pamoja na Kamati ya ufundi na kuweka wazi kuwa baada ya msimu huu kumalizika ili wajue ni sehemu gani za kupaboresha.
“Ninaomba wanasimba wasiwe na wasiwasi msimu ujao tutafanya mabadiliko ambayo yatamwacha mdomo wazi kila mtu, tumedhamiria makubwa tunataka turudishe heshima yetu ya mwanzo,” amesema