Klabu ya Manchester United itakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Newcastle United katika mpango wao wa kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini England na klabu ya Crystal Palace Michael Akpovie Olise.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Sun, Manchester United ilikuwa klabu pekee iliyokuwa na lengo la kumsajili Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, na iliamini huenda ingempata kirahisi mwishoni mwa msimu huu, lakini sasa mambo yamebadilika.
Mapema leo Jumatano (Mei 09) gazeti hilo limeripoti kuwa Newcastle United pia wanamtaka Olise kwa dau la Pauni Milioni 60, ambaye alichagia ushindi wa Crystal Palace wa 4-0 dhidi ya Manchester United juzi Jumatatu (Mei 07).
Kwa mantiki hiyo Manchester United watalazimika kujifunga mkwiji ili kufanikisha mpango wao wa kuisaka huduma ya Olise kwa zaidi ya dau la Pauni Milioni 60, ambalo linatarajiwa kuwekwa mezani huko Selhurst Park na Newcastle United.
Gazeti la The Sun limeandika: “Manchester United imepata pigo kubwa katika harakati zake za kumsaka Michael Olise,”
“Hiyo ni baada ya Newcastle United kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kumnasa nyota huyo, huku The Magpies kuwa tayari kuliipa Crystal Palace Pauni Milioni 60, ili kumsajili Kiungo huyo mwishoni mwa msimu huu 2023/24.
“Olise alionyesha kwanini Manchester United wanahitaji kumsajili, kwa kuupiga mwingi na kufanikiwa kufunga mabao mawili wakati Palace ikiibanjua United mabao 4-0.
“Wamiliki wenza wa Manchester United ‘Ineos’ wameripotiwa kumfuatilia Olise, huku Sir Jim Ratcliffe akidhaniwa kuwa shabiki wa mchezaji huyo.
“Klabu nyingine inayotajwa kumuwania Olise ni Chelsea, lakini bado Palace inaonekana kuwa na ofa nzuri zaidi.”