Azam FC wataikaribisha Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam leo Alhamis (Mei 09).
Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza Uwanja wa CCM Kirumba ambao Simba SC walikuwa wenyeji, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 huku Azam FC wakitangulia kufunga kipindi cha kwanza bao la Prince Dube na Simba SC kusawazisha dakika za mwisho za kipindi cha pili mfungaji akiwa Clatous Chama.
Kwenye msimamo wa ligi, Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 57 katika mechi 25 ilizocheza na Simba SC ikishika nafasi ya tatu baada ya kukusanya alama 53 ikicheza michezo 24.
Mchezo wa leo Alhamis (Mei 09) ni muhimu kwa timu zote katika kuhakikisha zinapata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao 2023/24.
Ushindi kwa Azam FC utakuwa na tafsiri ya kuongeza tofauti ya alama dhidi ya Simba SC na kuwa saba.
Kama Wekundu wa Msimbazi wataibuka na ushindi, watakuwa wamepunguza pengo la alama na matajiri hao wa Jii la Dar es salaam wanaoshika nafasi ya pili.
Akizungumza kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry amesisitiza umuhimu wa waamuzi kuchezesha kwa haki kuzingatia sheria 17 za mchezo huo.
“Hofu yangu iko kwa waamuzi. Tunatarajia wachezeshe kwa haki mchezo huu na timu bora uwanjani iondoke na alama tatu,” amesema Ferry
Ferry ameshauri Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ kuleta Teknolojia ya Marejeo ya Video msimu ujao kuhakikisha haki inatendeka uwanjani.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda amesema anatambua ugumu wa mechi yao dhidi ya Azam FC lakini wana imani watapata ushindi kwenye mchezo huo.
“Tuna fahamu mechi yetu dhidi ya Azam FC itakuwa ngumu, lakini tumejiandaa vya kutosha kupata ushindi. Ninaamini kila mchezaji wetu atatimiza wajibu wake uwanjani,” amesema Mgunda
Mechi nyingine za leo ni Mtibwa Sugar dhidi ya Tabora United Uwanja wa Manungu, Ihefu dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Liti na Namungo dhidi ya Geita Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi.