Wakati Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wakisaka mrithi wa beki wao wa kushoto Joyce Lomalisa, mlinzi wa Saint-Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasía Congo (DRC), Chadrack Boka bado hajakubali kutia saini mkataba wa kukipiga katika timu hiyo.
Young Africans inahitaji saini ya beki huyo raia wa DRC, kuchukua nafasi ya Lomalisa ambaye anatarajiwa kutimka mwishoni mwa msimu huu.
Juma lililopita iliripotiwa kuwa klabu hiyo yenye maskani mtaa wa Twiga na Jangwani, haina nia ya kumwongeza mkataba Lomalisa ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Sababu ya Young Africans kutompa mkataba mpya beki huyo wa zamani wa Bravos do Maqui ya Angola ni kutokana na mlinzi huyo kukabiliwa na majeraha ya mara kwa mara.
Kufuatia hatua hiyo, Rais wa Young Africans, Mhandisi Hersi Said, mwishoni mwa juma lililopita alikwenda nchini DRC kufanya mazungumzo na Boka aliyebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa St. Lupopo kuangalia uwezekano wa kuinasa saini yake.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya Young Africans, Hersi alikutana na kuzungumza na Boka lakini mazungumzo hayo hayakufikiwa muafaka.
Chanzo kimeeleza kuwa mazungumzo kati ya Hersi na Boka yataendelea lakini pia Rais huyo atakutana na kufanya mazungumzo na klabu ya St. Lupopo kujua gharama za kuinasa saini ya mlinzi huyo.
“Mchezaji (Boka) bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu yake ya sasa, hivyo Hersi kazungumza na mchezaji lakini pia atatakiwa kukaa mezani kuzungumza na klabu yake,” kimesema chanzo hicho cha uhakika.
Mbali na suala hilo, Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA), alikutana na Rais wa TP Mazembe ya nchini humo, Moise Katumbi na kufanya naye mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo uendeshaji.
Kabla ya kwenda DRC, juma lililopita iliyopita Hersi aliweka wazi kuwa, atahakikisha msimu ujao wanapata wachezaji bora kufikia malengo watakayojiwekea.
“Katika usajili huu tutakuwa makini sana, kwanza tutahakikisha tunambakisha mchezaji ambaye yupo katika mipango ya kocha (Miguel Gamondi), ikishindikana tutahakikísha Young Africans inanufaika na kuondoka kwake.
“Kingine tutatafuta mbadala mzuri zaidi yake, naamini tukifanya hivyo usajili utakuwa bora na tutafikia malengo yetu,” Hersi alisema
Young Africans ambayo hivi sasa inaongoza msimanmo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 65 katika mechi 25, pia ipo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘CRDBFC’.
Timu hiyo pia, msimu huu iliishia katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL), ikitolewa na Mamelodi Sundowns kwa Penati 3-2 baada ya kutoka suluhu katika mechi zote mbili.