Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuziimarisha Taasisi za Ujenzi ili kuhakikisha wataalamu wazawa wanakuza taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Miradi inayojengwa na Watanzania.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwaendeleza wataalamu wa Usanifu, Uhandisi na Wakadiriaji Majengo Tanzania hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Maonesho Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Amesema, Serikali zote mbili zimetoa kipaombele kwa wataalamu wa Ujenzi na Makampuni ya ndani ya nchi kupitia Wizara na Taasisi ambazo zimefanya jitihada maalum za kuweka Sera, Sheria na kanuni zenye vigezo rafiki ili kurahisisha maombi ya kazi za ujenzi hapa nchini.
Hemed amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuitumia vyema nafasi waliyoipata ili kuweza kupata uwelewa mkubwa na mbinu mbali mbali za ujenzi ikiwemo utumiaji wa njia mbadala ya vyuma hasa Zanzibar ambapo kumekuwa na uhaba mkubwa wa matumizi mali zisizorejesheka kama vile mchanga na nyenginezo.