Kumalizika kwa ujenzi wa daraja la Berega lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kumewaondolea adha wanawake na watoto ambao walikuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa mbele ya Rais Samia wakati wa ziara yake alipokuwa akizindua daraja hilo.
Amesema, daraja Daraja hilo ni kiungo muhimu sana kwa kuwa linaunganisha Mikoa miwili wa Morogoro na Tanga kwenye Wilaya ya Kilindi ambapo eneo hilo lilikuwa likikosa mawasiliano kwa mwaka mzima kutokana na maji kujaa na kusababisha wananchi kushindwa kuvuka upande wa pili kupata huduma za kijamii ikiwamo za afya.
“Kwa kipindi kirefu wananchi wamepata shida, wameshindwa kusafirisha bidhaa zao kwenda sokoni lakini wamepoteza maisha yao kutokana na maji kujaa msimu wa mvua na kupelekea wananchi wa Kilosa na Kilindi kushindwa kuwasiliana na kukosa fursa za msingi za kibiashara, kijamii na kiafya,” alisema Mchengerwa.