Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamekwama kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo baada ya kutoka sare tasa nyumbani juzi, Jumamosi dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kufikisha pointi nane ambazo hazikutosha kuiwezesha kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa kundi A ambazo zingeipa tiketi ya kucheza robo fainali.

Timu mbili zilizofuzu katika kundi la Yanga ni Al Hilal ya Sudan ambayo imemaliza ikiwa inaongoza na pointi 10 pamoja na MC Alger ambayo imeshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa na timu nyingine kwenye kundi hilo, TP Mazembe iliungana na Yanga kuaga baada ya kushika mkia.

Kutolewa huko maana yake kumeifanya Yanga ishindwe kurudia ilichokifanya msimu uliopita ambapo ilitinga hatua ya robo fainali na kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya timu hizo kutoka sare tasa kwenye mechi mbili baina yao.

Ifuatayo ni tathmini ya namba kwa mambo tofauti yahusuyo Yanga katika mashindano hayo ambayo yana hadhi ya juu zaidi kwa soka la ngazi ya klabu barani Afrika.

01. Idadi ya michezo ya hatua ya makundi ambayo Yanga imepata ushindi katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo pekee ambao Yanga imepata ushindi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ni dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo ambao iliichapa timu hiyo ya DR Congo kwa mabao 3-1, Januari 4 mwaka huu.

Imetoka sare moja na kupoteza moja nyumbani hivyo kuifanya ipate pointi nne tu kati ya tisa ilizopaswa kuvuna katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

08. Pointi nyingi ambazo Yanga imewahi kukusanya katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni nane ambazo imezipata msimu huu na pia ilipata idadi kama hiyo ya pointi msimu uliopita.

Msimu uliopita ilifuzu robo fainali ikiwa na pointi hizo nane lakini awamu hii haikufanikiwa kusonga mbele.

06. Yanga imeshiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika mara tano ambapo mara tatu ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mara mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mara hizo sita, ni mara mbili tu ambazo iliweza kusonga mbele kwenda robo fainali na mara nne ilikwama katika makundi.

02. Clement Mzize na Stephane Aziz Ki kila mmoja amefunga mabao mawili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika yote akipachika katika mchezo wa raundi ya nne dhidi ya TP Mazembe ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mabao hayo yanawafanya Mzize na Ki kuwa wachezaji walioifungia Yanga mabao mengi kwenye hatua hiyo msimu huu huku bao lingine moja likifungwa na Prince Dube.

44. Asilimia ya mashuti yaliyolenga lango ambayo Stephane Aziz Ki amepiga katika mechi sita za hatua ya makundi akiwa ndiye mchezaji anayeongoza kwa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango katika kikosi cha Yanga akiwa na wastani wa mashuti 2.3 kwa mechi.

362. Wastani wa pasi zilizopigwa na Yanga kwa mchezo kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika msimu huu sawa na asilimia 80.2.

Pasi hizo zinaifanya Yanga ishike nafasi ya nne katika chati ya timu zilizopiga pasi sahihi nyuma ya Mamelodi Sundowns, Al Ahly na Pyramids FC.

09. Idadi ya nafasi za mabao ambazo Yanga imepoteza katika mechi sita za hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya MC Alger, Al Hilal na TP Mazembe.

04. Wastani wa krosi ambazo Yanga imepiga kwa mechi katika hatua ya makundi ikiwa ni sawa na asilimia 22.4.

Yanga imemaliza hatua ya makundi ikiwa inashika nafasi ya sita katika chati ya timu ambazo zina wastani mzuri wa kupiga krosi kwa mechi.

Timu tano zilizo juu ni Pyramids FC, Maniema, Esperance, Djoliba na CR Belouizdad.

48. Idadi ya kona 48 zimepigwa na Yanga katika mechi sita ambazo imecheza kwenye kundi lake.

Kwa wastani, Yanga katika kila mechi moja ya hatua ya makundi msimu huu ilipata kona nane.

13. Djigui Diarra anashika nafasi ya 13 katika chati ya makipa waliookoa hatari nyingi kwenye hatua ya makundi ambayo inaongozwa na Ayoub El khayat wa FAR Rabat ya Morocco.

Diarra ameokoa asilimia 60 za hatari ambazo Yanga ilielekezewa langoni mwake.

Majaji wa Mahakama ya Rufani wala kiapo Ikulu
Maisha: Hata kama ni ndoa sio kwa mume huyu