Rais mteule wa Marekani, Donald Trump kwa mara ya kwanza ameigeukia Urusi na kueleza kuwa anaamini nchi hiyo ilihusika kufanya udukuzi dhidi ya Democratic wakati wa harakati za uchaguzi wa mwaka jana.
Trump aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari uliokuwa wa kwanza ‘rasmi’ na wanahabari tangu atangazwe kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic.
Hata hivyo, Trump alieleza kuwa ingawa anaamini kuwa Urusi ilihusika kufanya udukuzi huo katika ‘compyuta’ za Democratic, nchi hiyo haikufanya lolote kwa lengo la kumsaidia yeye kushinda uchaguzi.
Bilionea huyo ameeleza kuwa ingawa kitendo hicho anaamini kilifanywa na mashushu wa Urusi, hakitajirudia tena wakati wa utawala wake.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Barack Obama aliagiza kitengo cha usalama kufanya uchunguzi wa haraka kubaini kama Urusi ilihusika kufanya udukuzi kuingilia uchaguzi wa Marekani. Kitengo hicho kimekuwa kikieleza kuwa Urusi walihusika moja kwa moja lakini bado hakijawasilisha ripoti kamili ya uchunguzi huo.
Hata hivyo, Serikali ya Urusi imekanusha vikali taarifa hizo za Marekani na kudai kuwa zimetengenezwa.
Trump amekuwa akionesha urafiki wa wazi na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hali inayokosolewa vikali kuwa ni kinyume cha sera na msimamo wa Marekani. Trump amekuwa akisisitiza kuwa atashirikiana na Urusi kupambana na kundi la kigaidi linalojiita Islamic States of Iraq and Syria (ISIS).