Baada ya kupokea kipondo cha mabao manne kwa sifuri kutoka kwa Everton katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England, meneja wa klabu ya Man city Pep Guardiola, amekubali kuwa katika wakati mgumu wa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa kwa msimu huu wa 2016/17.
Guardiola aliafiki suala hilo, alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mtanange huo kumalizika katika uwanja wa Goodison Park huko mjini Liverpool.
Guardiola aliwaambia wandishi wa habari kuwa, ni wakati mgumu sana kwake kukubali kuendelea kuwa katika ushindani wa kuwania ubingwa wa PL kwa msimu huu, kutokana na uwiyano wa point uliopo dhidi ya vinara Chelsea.
Alisema, kuwa nyuma kwa point 10 dhidi ya anaeongoza ligi ni mtihani mkubwa sana kwa timu ambayo inahitaji kutwaa ubingwa, hivyo hana budi kukubali yupo katika wakati mgumu wa kupambana na kufikia malengo.
“Mara kadhaa nimekua ninazungumza na wachezaji wangu kuhusu ushindani wa ligi, na huwa nawataka wasahau kuhusu muonekano wa msimamo wa ligi, naamini wakifuatilia suala hilo litawachanganya na watashindwa kushindana.”
“Tunapaswa kujiwekea mipango ya kushinda kwanza na suala la mtazamo wa msimamo wa ligi lije baadae, ndio kama mlivyoona kwa msimu huu imedhihirisha msimamo sio lolote sio chochote kwetu, maana hautusaidii zaidi ya kuangalia ni vipi tunashindana yoyote atakaekua mbele yetu.” Alisema Guardiola.
Mabao ya Everton katika mchezo wa jana yalifungwa na Romelu Lukaku aliyefunga mawili, Kevin Mirallas na Tom Davies katika dakika ya 34,47,79 na 90.