Mamlaka ya Bandari nchini imeshauriwa kubuni utaratibu wa kurasimisha bandari bubu ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazopitishwa katika maeneo hayo zinakubalika kisheria.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri wakati  timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango ilipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kufanya ufuatiliaji na tahmnini ya shughuli zinazotekelezwa bandarini hapo.

Mwanri amesema kurasimisha bandari bubu kwa sasa ni muhimu kwa sababu karibia maeneo yote nchini kuna bandari za aina hiyo, ambapo Mkoa wa Tanga peke yake una bandari kama hizo takribani 42, ambazo zinaendesha shughuli mbalimbali bila  ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari.

“Kuna umuhimu mkubwa kuangalia shughuli zinazoendelea katika bandari bubu kwa kuwa wakati mwingine wafanyabiashara wanapaswa kulipa kodi wanatumia maeneo hayo kupitisha bidhaa bila kulipa kodi na wengine wanatumia bandari bubu kuendesha biashara haramu. Ni lazima kuanza kufanya utaratibu wa kurasimisha bandari hizo ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu,” alisema Mwanri.

Hata hivyo, Mwari ametembelea maeneo ya Bandari ya Tanga na kushuhudia shughuli mbalimbali zikiendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa gati namba 2 ikiwa ni moja ya malengo katika kuimarisha huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Bandari hiyo Saleh Sapi, amesema kuwa Bandari ya Tanga inapokea tani laki mbili za mizigo kwa mwezi ambapo  bidhaa kubwa zinazoingizwa kutoka nje ni malighafi ya kutengenezea saruji wakati bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ni kahawa, mkonge, pamoja na mbao ambazo kwa sasa kibali chake kimesitishwa kwa muda.

 

Simbu aitoa kimasomaso Tanzania katika mashindano ya riadha
Pep Guardiola Akiri Maji Kumfika Shingoni