Wagogo ni moja ya makabila makubwa Tanzania, wenyeji wa mikoa ya Dodoma na Singida. Wagogo walikuwa wakiongozwa na mtu aliyeitwa Mtemi. Watemi kadhaa waliongoza kabila hilo kabla ya mfumo wa uongozi kuvurugwa na ukoloni ambapo Mtemi wa mwisho aliitwa Mazengo ambaye alitokea katika kijiji cha Mvumi, wilaya ya Dodoma vijijini.
Wagogo wamekuwa wakijenga nyumba ambazo kwa Kigogo huitwa “itembe”. Tangu zamani kuta za tembe zilijengwa kwa fito (kwa Kigogo hutamkwa sito) zilizosukwa kwa kupisha kuzuia mwanga na maji.
Vipande vya kuta vilivyosukwa kwa sito vinaitwa “izizi”.
Tembe huezekwa kwa udongo ambao hushikiliwa na miti midogomidogo iitwayo “walo”. Walo huwa inashikiliwa na miti mikubwa kidogo iitwayo “mahapa” na mahapa hushikiliwa na miti mikubwa iitwayo “michichi”. Michichi ambayo ndiyo hubeba uzito wote hushikiliwa na nguzo kubwa za miti imara na migumu. Nguzo hizo hutiwa “masumbilili”.
Kwa miaka ya karibuni kuta za tembe hujengwa pia kwa matofali yanayotengenezwa kwa udongo.