Kocha kutoka nchini Ufaransa Michel Dussuyer ametangaza kujiuzulu kukifundisha kikosi cha timu ya taifa ya Ivory Coast, ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa kwenye fainali za Afrika za mwaka huu 2017 (AFCON 2017).

Dussuyer mwenye umri wa miaka 57, anakua kocha wa pili kutangaza kujiuzulu kwa sababu za kushindwa kufikia malengo kwenye fainali za Afrika zinazoendelea nchini Gabon, akitanguliwa na Georges Leekens aliyekua anakinoa kikosi cha Algeria.

Dussuyer ametangaza Kung’atuka, baada ya kuwa kocha mkuu wa kikosi cha Ivory Coast kwa kipindi cha miezi 18, ambapo katika kipindi cha utawala wake alifanikisha safari ya Tembo hao wa Afrika ya Magharibi kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka huu.

Kupoteza mchezo dhidi ya Morroco, siku ya jumanne ya juma lililopita ilikua shubiri kwake na aliona hapaswi kuendelea kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Ivory Coast, baada ya kushindwa kuiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wa Afrika.

“Nimechukua maamuzi haya baada ya kukaa chini na viongozi wa shirikisho la soka nchini Ivory Coast na kukubaliana kwa dhati, ninamshukuru kila mmoja aliyefanikisha kazi yangu tangu nipofika hapa, Ninaitakia kila la kheri Ivory Coast pamoja na atakaerithi nafasi yangu.” Ilieleza taarifa ya kocha huyo ambayo ilitolewa na shirikisho la soka nchini Ivory Coast.

Dussuyer tayari ameshiriki mara tano katika fainali za Afrika akiwa na timu za mataifa matatu tofauti, Guinea mara tatu, Benin mara moja na Ivory Coast Mara moja.

Video: Waliofukiwa siku 3 mgodini wasimulia, Maalim Seif: Nitakuwa Rais Z'bar
Olympic Marseille Wamrudisha Dimitri Payet