Hatimae kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Dimitri Payet amefanikisha mpango wa kuachana na wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd), kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili.

Payet ambaye aliingia katika mzozo na meneja wa West Ham Utd Slaven Bilic baada ya kugomea mazoezi ya kikosi cha kwanza cha klabu hiyo kwa shinikizo la kutaka kuuzwa katika kipindi hiki cha mwezi januari, amejiunga na klabu ya Olympic Marseille inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa (Ligue 1).

West Ham Utd wamekubali kumuachia Payet kwa dau la Pauni milioni 25 na kumaliza mzozo wa kiungo huyo ambao ulifika mbali zaidi, hadi kutokua na mahusiano mazuri na wachezaji wenzake wa kikosi cha kwanza.

Payet amesaini mkataba wa miaka minne na nusu baada ya kufanyiwa vipimo vya afya mapema jana, na hii leo atatambulishwa kwa waandishi wa habari itakapofika michale ya saa saba na nusu mchana kwa saa za England.

Katika utambulisho huo, Payet ataongozana na rais wa klabu ya Olympic Marseille Jacques-Henri Eyraud pamoja na mkurugenzi wa michezo Andoni Zubizarreta.

Payet aliondoka Marseille na kujiunga na Wagonga nyundo wa jijini London mwaka 2015, na aliisaidia klabu hiyo ya jijini London kupambana vilivyo kwenye ligi ya nchini England hadi kumaliza msimu wakiwa katika nafasi ya saba.

Akiwa nchini England alikaribia kutajwa mchezaji bora wa msimu kupitia chama cha wachezaji wa kulipwa (PFA), lakini kura zake hazikutosha na badala yake alitangazwa Riyad Mahrez kuwa mshindi.

Ameondoka London Stadium huku akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 48 na kufunga mabao 11.

AFCON 2017: Michel Dussuyer Ang'atuka
Anglikana kwazidi kufukuta,Askofu Mokiwa atishia kupasua jipu