Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutambua mchango mkubwa wa aliyekuwa mwandishi mashuhuri wa Kiswahili, Shaaban Robert alitunga shairi la maombolezo yake mara tu baada ya kifo cha mashuhuri huyo aliyefariki dunia huko Tanga Juni 22, 1962.
Mwalimu Nyerere aliandika hivi:-
Twalia sote twalia, Kwa kufiwa Shaabani,
Majonzi kutuachia, Wa bara na Pwani,
Lugha alitupambia, Kwa vina na kwa mizani,
Nani hakumsifia?
Na lugha endeleeni, Kuipamba isifike,
Ipambeni kwa mizani, ipendeze isifike,
Pembe zote duniani, Isomeke iimbike,
Mwalimu wetu Shaabani, Naye pia atukuke,
Watungaji mlobaki, Mtampa tuzo gani,
Twajua mali hataki, Mali ‘taitakiani,
Basi mwombeni Maliki, Mtunza wema, Manani,
Bwana, agawaye haki, Amweke pema Shaabani.
Shaaban Robert alikuwa na mchango kubwa sana katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee, East Africa Literature Bureau na Tanganyika Languages Board.
Aliandika vitabu ishirini na mbili, kama Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu.
Shaaban Robert alifariki dunia huko Tanga tarehe 22 Juni 1962 akazikwa Machui.