Shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF) limetangaza kumuunga mkono mpinzani wa Rais wa CAF Issa Hayatou kuelekea uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao mjini Adis Ababa- Ethiopia.
Hayatou anawania kiti cha uraisi kwa mara ya nane mfululizo, baada ya kuingia madarakani mwaka 1998, na tayari amepata mpinzani kutoka Madagascar Ahmad Ahmad, ambaye anaungwa mkono na mataifa ya kusini mwa Afrika COSAFA.
Rais wa shirikisho la soka nchini Nigeria Amaju Pinnick, ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC kuwa, NFF inamuunga mkono Ahmad Ahmad.
Amesema Ahmad ni mtu aliyeonyesha ujasiri na kujitokeza hadharani kwa lengo la kumpa upinzani Issa Hayatou, na NFF inaamini kiongozi huyo wa chama cha soka nchini Madagascar anaweza kuwa dira mpya katika soka la Afrika.
Pinnick amesema CAF inahitaji kuwa na changamoto mpya ya uongozi, baada ya kuongozwa na Hayatou kwa kipindi kirefu kilichopita.