Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wana matumaini makubwa ya kukamilisha dili la kumsajili aliyekua mshambuliaji wa pembeni wa Arsenal Serge Gnabry, ambaye kwa sasa anaitumikia Werder Bremen.
Jarida la Kicker limeandika mpango huo wa The Bavarians, ambao wanaamini mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ana vigezo vya kuwatumikia kuanzia msimu ujao wa ligi.
Tangu aliporejea moja kwa moja nchini Ujerumani, Gnabry ameshaitumikia Werder Bremen katika michezo 21 na kufunga mabao 10.
Mwenendo huo kwa Gnabry, umekua kivutio kwa viongozi na benchi la ufundi la Bayern, hali iliyosababishaa kuanza kumfuatilia.
Hata hivyo nchini Hisapnia jarida la Sport limeripoti kuwa, FC Barcelona nao wameonyesha dhamira ya kutaka kumsajili mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huu, hivyo huenda Bayern Munich wakapata upinzani.
Gnabry aliondoka Arsenal baada ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza na alilazimika kupelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya West Brom msimu wa 2015-2016, kabla ya kuuzwa Werder Bremen kwa ada ya Pauni milioni 5.
Kabla ya hapo Gnabry aliwahi kucheza soka nchini kwao Ujerumani katika timu za vijana za TSV Weissach (1999–2000), GSV Hemmingen, (2000–2001), TSF Ditzingen (2001–2003), SpVgg Feuerbach (2003–2005), Stuttgarter Kickers (2005–2006) na VfB Stuttgart (2006–2011).