Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini inayofanyika nchini kwa sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.

Amesema ukiukwaji huo unachangia kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada hata kama kuna vito viliyokakatwa au havijakatwa.

Majaliwa amesema hayo wakati akihitimisha kikao alichokiitisha kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam kilichojumuisha Mawaziri wa Fedha pamoja na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo.

Amesema licha ya kuwa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili Serikali iweze kunufainika na madini hayo.

“Uzoefu wa kwenye minada ya korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima. Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,” alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa madini na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa bei inapaswa kuwa juu ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.

Majaliwa amemuagiza Kaimu Kamishna wa Madini, Benjamini Mchwampaka (ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Madini) aende Mererani na kufuatilia utendaji kazi wa mgodi wa Tanzanite One na suala zima la teknolojia zinazotumika kiwandani hapo.

Kikao hicho ni kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mererani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara Februari 16, 2017 kwamba akimaliza ziara ya mkoa huo ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite One baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi sasa.

Majaliwa amemwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa ndege vya Arusha na Kilimanjaro (KIA), ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini unaongezeka.

“Kamishna wa TRA na watu wako inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi zinafanyika kwenye sekta ya madini wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo. Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri waje kuwaletea malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija wakakuta mmetoka ofisini je?” amehoji Majaliwa.

 

Serge Gnabry Awindwa Allianz Arena
Video: Waziri Nape - Nitajiuzulu, Siku 30 zitakavyotikiswa na matukio matano nchini