Meneja wa magoo wa jiji (Liverpool) Jurgen Klopp ameahidi kufanya mazungumzo na mshambuliaji Daniel Sturridge itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Klopp atafanya mazungumzo hayo ili kujua mustakabali wa mshambuliaji huyo ambae juzi alikosa kujumuika na wenzake wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England, ambao ulimalizika kwa Liverpool kuambulia kibano cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa mabingwa watetezi Leicester City.
Sturridge mwenye umri wa miaka 27 alikosa mchezo huo kufuatia kuwa majeruhi, hali ambayo inaendelea kumuweka katika mazingira magumu ya kubaki klabuni hapo.
Mpaka sasa Sturridge ameshafunga mabao mawili katika michezo ya ligi aliyocheza msimu huu, huku wachezaji wenzake wanaocheza nafasi ya ushambuliaji wakionyesha juhudi na kufunga mabao zaidi.
Klopp tayari ameshaweka wazi kuwa, mwishoni mwa msimu huu atafanya marekebisho ya kikosi chake kwa kukubali kuwaachia baadhi ya wachezaji waondoke na kuwasajili wengine, baada ya kuona mapungufu ambayo yanaendelea kuwanyima nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu.
“Nitafanya jambo mwishoni mwa msimu huu, ili kukiboresha kikosi cha Liverepool. Nitazungumza na wachezaji wote akiwepo Daniel lakini haimaanishi kama ninamuondoka katika mipango yangu ya sasa,”
“Daniel hajafanya mazoezi kwa siku nane ama tisa hivi kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili. Tutajaribu kumsaidia ili kumuwezesha arejee kwenye kiwango chake cha kawaida, lakini mwishoni mwa msimu huu tutafanya njia mbadala ya kuzungumza nae. Alisema Klopp.
Mwishoni mwa juma hili Liverpool watakuwa wenyeji wa washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London Arsenal, na kama watafanya vibaya wataendelea kupoteza malengo ya kutwaa ubingwa.
Katika mchezo wa kwanza Liverpool waliifunga Arsenal mabao manne kwa matatu kwenye uwanja wa Emirates jijini London.