Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (TABOA) kwa kushirikiana na Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Dar es Salaam kimetangaza mgomo wa usafirishaji abiria na mizigo nchi nzima ili kushinikiza Serikali kutopitisha sheria ya usafirishaji inayotarajiwa kupitishwa siku ya Jumanne
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Eneo Mrutu amesema kuwa sheria hiyo mpya inayotarajiwa kupitishwa haikuwashirikisha wadau na haitenganishi makosa ya dereva na mmiliki wa chombo cha usafirishaji ambayo inapelekea mmiliki kufungwa jela.
“Abiria watuwie radhi, lakini watambue kuwa athari watakazopata zinatokana na sheria kandamizi inayotaka kutungwa na Sumatra kuwakandamiza wenye mabasi na daladala, sheria hii ikipita hakuna mmiliki wa basi atakaye endelea na biashara hii, hivyo kwa sauti moja tumeamua kugoma ili kupaza sauti,”amesema Mrutu.
Aidha, Mrutu amewataka wabunge bila kujali itikadi zao kutopitisha sheria hiyo hadi itakapobadilishwa na kushirikisha wadau kwakuwa inalenga kuharibu sekta ya usafirishaji nchini.
Hata hivyo, mgomo huo unatarajia kuanza leo jumatatu ili kushinikiza kutopitishwa kwa mswaada huo wa sheria ambao utawabana wamiliki na madereva pindi litokeapo tatizo.