Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imefuta kesi iliyokuwa inamkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ya kumtolea lugha chafu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Saalam, Kardinali Polycarp Pengo.
Uamuzi wa kufutwa kesi hiyo umetolewa na Hakimu wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha baada ya upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, kuomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa hawakuwa na shahidi wa pili. Upande wa Jamhuri umeleta shahidi mmoja pekee ndani ya kipindi cha miezi 14.
Hakimu Mkeha alitumia kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kufuta kesi dhidi ya kiongozi huyo wa dini.
Katika kesi ya msingi, Askofu Gwajima ambaye alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 17 mwaka 2015 anadaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Kardinali Pengo kati ya Machi 16 na 25 mwaka 2015, akiwa katika viwanja vya Tanganyika Packers vilivyoko Kawe jijini Dar es Salaam.