Mgombea urais wa Kenya kwa tiketi ya umoja wa vyama vya upinzani wa NASA, Raila Odinga ameweka wazi ombi lake kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa kuhusu mchakato wa uchaguzi huo.
Amesema kuwa Lowassa pamoja na Rais John Magufuli waliochuana kwenye uchaguzi mkuu uliopita ni marafiki zake, na kuwaomba wote wamuunge mkono kwenye uchaguzi huo.
Ombi la mwanasiasa huyo mkongwe wa Kenya na Waziri wa zamani wa nchi hiyo limekuja siku chache baada ya Lowassa kuweka wazi kuwa atamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta ili aendelee kuitawala nchi hiyo.
“Mimi na familia yangu tunamtumikia Mungu lakini vilevile kwa dhati kabisa sisi wana Monduli tunamuunga mkono Uhuru Kenyatta kwenye mbio za Urais nchini Kenya. Naomba nitamke wazi na dunia yote ijue kuwa sisi tunampenda Uhuru Kenyatta naye anatupenda, kwa hiyo tunamuunga mkono kwa kuwa tunaamini ana uwezo wa kuwaunganisha Wakenya na Watanzania,” alisema Lowassa alipotembelewa na wabunge wanawake kutoka Kenya, nyumbani kwake Monduli takribani mwezi mmoja uliopita.
Lowassa ana ushawishi kwa kiasi fulani kwenye uchaguzi huo kwa kuwa ni kiongozi mkuu wa Wamasai (Leigwanan) katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo pia kimeweka wazi kuwa kitamuunga mkono Kenyatta kwa kuwa kinaridhika na namna alivyofanya kazi hususan kuruhusu demokrasia nchini kwake.
Hata hivyo, msemaji wa vyama vya upinzani nchini Kenya, Philip Etale alisema kuwa Odinga ni rafiki wa Lowassa na Magufuli na kwamba asingependa urafiki huo upotee kwa sababu za kisiasa.
“Odinga aliweka bayana wakati wa kampenzi za uchaguzi wa Tanzania kuwa anawaunga mkono wote na kutaka mgombea bora ashinde. Kama ODM tunaamini katika demokrasia na tusingependa wakati wowote ule, tupoteze marafiki zetu kwa sababu ya siasa,” ujumbe wa Etale unakaririwa na Mwananchi.
Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu, uchaguzi ambao unatajwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi kwani katika uchaguzi uliopita, Kenyatta na Odinga walizidiana kwa kiasi kidogo cha kura.