Mahakama ya juu ya India imefuta sheria iliokuwa inatumika nchini humo kwa wanaume kuwapa talaka wake zao kwa kusema tu neno talaka (talaq) mara tatu hata kwa njia ya simu.
Jopo la majaji watano lililofanya uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na wanawake watano nchini humo waliokuwa wametalakishwa kwa kuambiwa ‘talaka’ mara tatu, limeitangaza sheria hiyo kuwa kinyume na katiba na Uislamu.
Zakia Soman ambaye ni mmoja wa wanawake waliofungua kesi hiyo mahakamani hapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ushindi huo ni ushindi kwa wanawake wote nchini India kwani kwa miaka zaidi ya 70 wamekuwa wakinyanyaswa kwa kuachwa na wanaume wao kwa mtindo huo.
“Ni siku ya kihistoria kwetu. Lakini haiwezi kuishia hapa. Siwezi kueleza ni kwa kiasi gani wanawake wa India walionyanyasika kwa muda mrefu walivyotuunga mkono bila kujali imani zao na dini zao,” alisema Zakia Soman.
- Tanesco kuwashughulikia wafanyakazi wahujumu
- Jay Moe na Madee watoa somo kwa nyimbo zinazotoka hivi sasa
Katika kipindi cha hivi karibuni, imeripotiwa kuongezeka kwa talaka zinazoitwa ‘triple talaq’ (talaka tatu) zinazotolewa na wanaume kwa kuandika barua, kuwapigia wake zao simu, kutumia Skype, na hasa kutumia mtandao wa WhatsApp.
Ingawa mtindo huu umekuwa ukitumika kwa miaka mingi, Mahakama imeeleza kuwa hakuna sehemu yoyote kwenye Sheria za Kiislam au hata kwenye Koran Tukufu ambapo talaka tatu zimetajwa.
Viongozi na wakufunzi wa imani ya dini ya Kiislam wamesema kuwa Koran Tukufu imeeleza wazi kuwa kwa masuala ya talaka, inapaswa kupita kipindi cha miezi mitatu ili kuwapa nafasi wanandoa hao kufanya mazungumzo na kujaribu kurejesha mahusiano yao.