Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mifumo ya mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko ya hali ngumu ya maisha inayowakabili wazee waliostaafu na wananchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa hii leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mtambnile, Masoud Abdallah Salim (CUF).

Amesema kuwa Serikali inaboresha mifumo ya kukusanya mapato pamoja na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuleta unafuu wa maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.

Aidha, ameongeza kuwa, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya  usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya, elimu na kiuchumi hususan katika ukusanyaji mapato kwa lengo la kuboresha maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.

“Tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao ndio msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali,”amesema Dkt. Kijaji.

Hata hivyo, ameongeza kuwa maboresho ya viwango vya pensheni kwa Wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya Wastaafu hivyo Serikali imelenga zaidi kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii ili kupunguza malalamiko hayo.

 

Ufahamu zaidi ugonjwa wa kiharusi na tahadhari zake
Dirisha la usajili Uturuki kumuokoa Jack Wilshere