Watu sita wamejeruhiwa vibaya kwa kushambuliwa na tindikali katika jiji la London nchini Uingereza usiku wa kuamkia leo.
Jeshi la polisi jijini humo limeeleza kuwa msamalia mwema aliwapigia simu kuhusu tukio hilo majira ya saa mbili usiku katika eneo la Stratford Center mkabala na Westfield.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu waliojeruhiwa walikuwa katika makundi tofauti hali inayozua wasiwasi kuwa mshambuliaji au washambuliaji walilenga watu bila mpangilio.
Aidha, Jeshi hilo limesema linamshikilia mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 15 kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo.
“Kwa uchunguzi wa awali, na kwa kuzingatia ushambuliaji wa bila kufuata mpangilio tumebaini kuwa tukio hili limeyahusisha makundi mawili ya wanaume,” limeeleza tamko la Polisi.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni Meneja wa mgahawa wa Burger King aliyejitambulisha kwa jina la Hossen, aliiambia BBC kuwa baadhi ya majeruhi wa tukio hilo walikimbilia kwenye mgahawa wake kusafisha nyuso zao kwa maji.