Mbunge wa Singida Mashariki anayeendelea kupata matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya, amenena kuhusu tamko la Serikali kwa familia yake kuwataka kuandika barua kama wataridhia Serikali imsafirishe mbunge huyo kokote duniani kupata matibabu zaidi.

Kaka yake Lissu, Alute Mughwai amesema kuwa wao kama familia walijadiliana na mbunge huyo kuhusu tamko hilo na akawataka kutofanya lolote kwa wakati huo kwani atalizungumzia yeye mwenyewe.

“Lissu alitujibu kwamba suala hilo atalizungumzia yeye mwenyewe siku za hivi karibuni. Kwasababu yeye anaamini yeye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana haki zote ikiwa ni pamoja na akiugua au akipata maradhi,” Kaka yake Lissu aliiambia Azam TV.

Katika hatua nyingine, familia hiyo imesema kuwa imeandika barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuomba uchunguzi wa shambulio la mbunge huyo ufanywe na vyombo kutoka nje ya nchi.

“Lissu alipigwa risasi mchana kweupe, sasa mazingira hayo yametupa wasiwasi kama tukio hilo litachunguzwa kikamilifu. Hatuna wasiwasi na uwezo wa Jeshi letu la Polisi kufanya huo uchunguzi, wasiwasi wetu ni utayari wa jeshi letu kufanya hivyo,” alisema Mughwai ambaye ni msemaji wa familia hiyo.

Aliongeza kuwa nakala ya barua hiyo iliyoandikwa Septemba 16 mwaka huu imetumwa kwa waziri wa sheria na katiba.

Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lake nyumbani kwake eneo la Area D mjini Dodoma, mapema mwezi huu.

Jeshi la Polisi limeendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwataka watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia upelelezi kuziwasilisha kwa njia ya siri au njia ya wazi.

Sita washambuliwa kwa tindikali
Morata apiga hat-trick Chelsea ikiichapa Stoke City