Spika wa Bunge la Ethiopia, Abadula Gemeda amejiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni siku mbili kabla ya kufunguliwa kwa vikao vya bunge hilo.
Kwa mujibu wa tovuti maarufu ya Addis Standard, Gemeda amechukua uamuzi huo wikendi iliyopita kama ishara ya kupinga vitendo vya Serikali ya nchi hiyo katika masuala ya ulinzi kwenye majimbo ya Oromia na Somali.
Sababu kuu imeelezwa kuwa ni ukosoaji wa namna ambavyo Serikali inavyotumia vikosi vya ulinzi katika maeneo hayo wakati ambapo watu 50 wameripotiwa kufa na zaidi ya watu 150,000 wamepoteza makazi kutokana na mgogoro wa rasilimali unaohusisha ukabila.
Kabla hajawa Spika wa Bunge hilo tangu mwaka 2010, Gemeda aliwahi kuwa Gavana wa jimbo la Oromia na pia Waziri wa Ulinzi.
Spika mpya wa Bunge hilo anatarajiwa kuchaguliwa mara tu wabunge watakapokutana wiki hii.