Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans wanafikiria kumruhusu mshambuliaji wao Matheo Anthon kuondoka kwa mkopo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, baada ya kupokea maombi kutoka kwa Lipuli FC yenye maskani yake makuu mjini Iringa.
Kocha Selaman Matola, anaekinoa kikosi cha Lipuli FC kinachoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu huu wa 2017/18, amekua mstari wa mbele kuhakikisha suala la mshambuliaji huyo linakamilishwa katika kipindi hiki, ili kukiongezea nguvu kikosi chake ambachgo mwishoni mwa juma hili kitacheza dhidi ya Simba SC, katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Afisa Habari wa Young Africans, Dismas Ten amenukuliwa akisema benchi la ufundi likiongozwa na Kocha George Lwandamina bado halijapata jibu sahihi hadi sasa kuhusu suala hilo, lakini akasisitiza huenda jibu kamili likatoka wakati wowote kuanzia sasa.
“George Lwandamina ndiyo kocha mwenye kujua mapungufu ya timu yake na mahitaji hivyo sisi kama watendaji tumemfikishia mezani kwake na yeye ndiyo mwenye maamuzi ya kumruhusu au kumzuia Matheo kwenda Lipili FC,” amesema Ten.
Msemaji huyo pamoja na kukiri kuwa ni kweli mshambuliaji huyo anasota benchi lakini amesema endapo kocha atamruhusu wapo tayari kumpa baraka zote na wataitaka Lipuli kumtumia mchezaji huyo kwenye kikosi cha kwanza ili kumpa nafasi ya kupandisha kiwango chake.
Amesema mchezaji huyo bado ana mkataba mrefu, hivyo hatua ya kumpeleka Lipuli Fc kwa mkopo ni lazima akafanye kazi na kupandisha kiwango chake na siyo kukaa benchi kama iivyo sasa.
Tangu kuanza kwa msimu huu Matheo hajaitumikia Young Africans hata mechi moja wa Ligi Kuu, huku tatizo kubwa linaloonekana ni ushindani uliopo kwenye nafasi za ushambuliaji ambapo kuna wachezaji wengi wanaocheza nafasi hiyo na wamejenga imani kwa kocha Lwandamina.