Mzunguuko wa  20 wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara unatarajia kuanza kesho kwa mchezo mmoja kuchezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo vinara wa Simba SC watakuwa wenyeji wa Stand United.

Kuelekea mchezo huo, Kocha msaidizi wa Timu ya Stand United, Athuman Bilal amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuikabili Simba SC na tayari kikosi kipo jijini Dar es Salaam kikiendelea na mazoezi.

Kocha huyo amesema kuwa Simba ni timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine, hivyo wako imara kukabiliana nayo kwa ajili ya kuchukua pointi tatu.

Kwa upande wa Simba kupitia kwa Afisa Habari wake, Haji Manara amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo huo muhimu kwa upande wao.

Manara pia amesema nyota wawili wa timu hiyo, Emmanuel Okwi na John Bocco ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuwepo kikosini endapo kocha ataamua kuwapanga.

Kikosi cha wekundu wa Msimbazi Simba SC baada ya kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mbao FC, kiliingia mafichoni kujiwinda na mchezo dhidi ya Stand United lengo likiwa ni kufukuzia kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa muda mrefu.

Simba SC inaingia kwenye mchezo dhidi ya Stand United ikiwa inaongoza ligi kwa alama 45 lakini kwa upande wa Stand United wao wako nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi msimu huu wakiwa wamejikusanyia jumla ya alama 20.

Nadal ajiondoa michuano ya wazi ya Mexico
Rais Karia aweka msisistizo bima kwa wachezaji