Baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la soka nchini TFF kutangaza kumfungia kifungo cha maisha Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo, Michael Richard Wambura, mtuhumiwa huyo ameibuka na kupinga maamuzi kwa kusema utaratibu haukufuatwa.
Akizungumza na Waandishi jijini Dar es Salaam leo, Wambura amesema Kamati ya Maadili imeendesha shauri juu ya tuhuma zake, kitu ambacho ni kinyume na taratibu hivyo uamuzi ambao umetolewa na TFF ni kinyume na katika ya Shirikisho hilo.
Aidha Wambura amesema ameshangazwa kuona suala lenye zaidi ya miaka 14 kuibuliwa wakati huu ambapo yeye amekuwa ni Makamu wa Rais kwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 80.
Vilevile ameeleza kuwa suala la kughushi nyaraka linapaswa kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi huku akisema Kampuni inayosemekana nimechukua hizo pesa ina Wakurugenzi, kwanini sasa wasiitwe kuhijiwa ili kujua kama ni kweli au la.
Kutokana na hayo kujitokeza, Wambura amesema kuwa siku zote wakati akiwa ofisini hakuwa kuelezwa kuhusiana na jambo hilo mpaka pale aliposafiri ndiyo limeibuka na hukumu kutoka bila kusikilizwa shauri lake.
Sanjari na hayo, Wambura anaamini kuwa jambo hilo limewekwa kimkakati na wala halina ukweli wowote, na yupo tayari kufungwa kama itabainika ni kweli, hivyo anasubiri barua rasmi ya kufungiwa kisha atajua kipi cha kufanya.
Kamati ya maadili ilitangaza kumfungia kupitia taarifa iliyosomwa hii le na afisa habari wa TFF Clifford Mario Ndimbo, kutokana na makosa matatu, moja ni Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) ambazo ni za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
Pili ni kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
Na Tatu, ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015.