Majogoo wa jiji Liverpool huenda wakashindwa kukamilisha dili la kumsajili beki wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Yerry Mina.
Beki huyo kutoka nchini Colombia amekua na wakati mgumu kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Barca, hali ambayo imemlazimu kusaka timu katika kipindi hiki cha dirisha la usajili, na klabu ya Liverpool ilikua ya kwanza kuonyesha nia ya kumsajili.
Klabu ya Real Betis inayoshiriki ligi ya nchini Hispania, imetajwa kuingilia dili hilo, na imeonyesha kuwa tayari kukamilisha harakati za uhamisho wa Mina kwa mkopo.
Hata hivyo mchezaji huyo ameonyesha kuwa tayari kubaki nchini Hispania, kutokana na kuzoea mazingira ya nchi hiyo, tofauti na kwenda katika nchi nyingine ambapo anaamini huenda akapata wakati mgumu kuendana na mazingira.
Sababu nyingine ya FC Barcelona kumuweka sokoni Mina, ni kufuatia harakati za kumsajili beki kutoka nchini Brazil na klabu ya Gremio Arthur, ambaye juma hili anatarajiwa kupimwa afya huko Camp Nou, baada ya kukamilika kwa mazungumzo baina ya viongozi wa klabu hizo.
Mina ameitwa kwenye kikosi cha Colombia kinachoshiriki fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi, na jana jumapili aliifungia timu hiyo bao la ushindi dhidi ya Poland na kufufua matumaini kwa taifa lake kusonga mbele kwenye hatua ya 16 bora.