Siku moja baada ya uongozi wa Young Africans kuthibitisha kuliandikia barua shirikisho la soka nchini TFF kulalamika vitendo visivyo vya kiungwana walivyofanyiwa wachezaji wao na wachezaji wa mahasimu wao, Simba SC wakati wa mchezo wa ligi kuu ulioungurua mwishoni mwa juma lililopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, afisa habari wa Wekundu hao Haji Sunday Manara amefunguka.
Manara amedai kuwa Young Africans ‘wamekurupuka’ kuliandikia shirikisho la soka nchini kwa madai ya kuwanyooshea kidole wachezaji wa Simba SC, huku akiwataka wajiridhishe kama kweli utovu wa nidhamu ulionyeshwa na James Kotei dhidi ya beki wa kushoto Gardiel Michael pekee yake.
Manara amemjibu afisa habari wa young Africans Dismas Ten akisema kwamba, hata wachezaji wa Young Africans walifanya matukio yasiyo ya kiungwana kwenye mchezo huo akitolea mfano kitendo cha beki Andrew Vincent ‘Dante’ kumpiga kichwa Nahodha wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
“Hatukuwa wajinga tulipoamua kukaa kimya, tumewasaidia wale waliokwenda kushitaki TFF na Bodi ya Ligi na hili pia walipeleke.
Yule karusha ngumi na huyu kapiga kichwa,”amesema Manara na kuongeza; “Tukemee vitendo vyote vya kihuni Uwanjani siyo vya Simba tu,”.
Hata hivyo Manara amesema, mchezaji anaporusha kichwa kwa mwenzake kwa dhamira ovu, haijalishi kimemuathiri kwa kiasi gani – lakini anastahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na dhamira pekee.
“Kama ilivyokuwa kwa Kotei, mliokwenda kumshitaki, sawa ni hivi, hatuungi mkono vitendo hivi na tunavikemea, ila tusiegemee upande mmoja, si Dante wala Kotei waliofanya sahihi, adhabu ikija ije kwa wote, wakiachiwa ni wote,”amesema Manara.
Jana, Msemaji wa Young Africans, Dissmas Ten aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa, wamelazimika kuyaripoti TFF baadhi ya matukio yaliyofanyika katika mchezo huo ili hatua zichukuliwe, akitolea mfano kitendo cha kiungo Mghana wa Simba SC, James Kotei kumpiga ngumi beki wao, Gardiel Michael na refa Jeonesiya Rukyaa wa Kagera hakuchukua hatua.