Rais John Magufuli ameweka mkazo wa sababu za kutosafiri mara kwa mara kwenda nje ya nchi na badala yake kutuma mawaziri kumuwakilisha.

Akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa sababu kuu ya kuacha safari hizo ni kuepuka matumizi makubwa ya fedha za umma.

Alisema kuwa kumtuma Waziri na wasaidizi wake nje ya nchi ni gharama kidogo ukilinganisha na gharama kubwa za safari ya Rais.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alimtuma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Augustine Mahiga kumuwakilisha katika kikao cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, uliofanyika New York nchini Marekani.

Rais Magufuli alimpongeza Dkt. Mahiga kwa kumuwakilisha vizuri kwenye mkutano huo pamoja na mikutano mingine ya kimataifa hivyo kusaidia kuokoa fedha za umma.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amewahi kusafiri kwenda Uganda (mara mbili), Rwanda, Kenya na Ethiopia. Bado hajatoka nje ya bara la Afrika.

Katika kipindi cha utawala wake, amechukua hatua za kupunguza matumizi ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti safari za nje za watumishi wa umma na kufuta wafanyakazi hewa.

Marais wengine ambao hawakuhudhiria mkutano huo wa Umoja wa Mataifa ni pamoja na Yoweri Museveni (Uganda), ambaye pia alitoa sababu za gharama kubwa ukilinganisha na dakika 15 anazopewa kuzungumza. Pia, Vladimir Putin (Urusi),  Xi Jinping (China) na  Narendra Modi (India).

Haji Manara ajibu tuhuma za utovu wa nidhamu
Ebitoke aondoka Timamu TV, afuta kila kitu