Kocha wa Viungo kutoka nchini Tunisia Adel Zrane amesema yupo tayari kurudi Simba SC endapo Uongozi wa Klabu hiyo utakua tayari kumrudisha.
Zrane ametoa kauli hiyo akiwa nchini Kuwait anakofanya kazi kwa sasa, akiwa na klabu ya Al-Wehdat inayonolewa na aliyekua Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes Da Rosa.
Zrane amesema anaipenda na kuithamini Simba SC kwa sababu aliishi kama nyumbani, hivyo ikitokea Uongozi unaonyesha nia ya kuhitaji huduma yake kwa mara nyingine hatosita kurejea Msimbazi.
Amesema kwa sasa yupo huru kufanya kazi na yoyote, lakini Simba SC anaipa kipaumbe na atajihisi furaha sana endapo atarudi Klabuni hapo kuungana na wachezaji ambao aliwapenda na kuwazoea.
“Sasa niko Huru Kusikiliza ofa kutoka klabu yoyote ila Simba SC ni kipaumbele changu Kama watanihitaji muda wowote niko Tayari sababu moyo Wangu ni Simba SC” Adel Zrane
Kocha Zrane aliondolewa Simba SC sambamba na Kocha Didier Gomez, baada ya klabu hiyo kushindwa kufuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana msimu uliopita na kuangukia Kombe la Shirikisho.
Mwingine aliyeondolewa Simba SC katika mkumbo huo ni Kocha wa Walinda Lango Milton Nienov ambaye kwa sasa yupo kwenye Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans.